Pemba kisiwa kilicho tengwa

Pemba kisiwa kilichotengwa tangu 1952
Fahamu mengi kuhusiana na Pemba kupitia mm mpemba halisi na mwana sanaa mchanga wa historia.
YAHYA ABDULLAH KHAMIS EL~NABAHANIY.


Pemba ni kisiwa kinachojulikana kwa
umaarufu kama "al'jazeera al'khadra",
yaani "kisiwa cha kijani" kwa lugha ya
Kiarabu; ni kisiwa kinachoelea
mashariki ya pwani ya Afrika kwenye
Bahari ya Hindi – ni takriban
kilometa hamsini kaskazini ya kisiwa
cha Unguja; na kilometa hamsini
mashariki ya Tanganyika. Pemba, kama
"kisiwa" kimetokea kuwa maarufu kwa
zao la karafuu na hata kupewa jina la
"kisiwa cha marashi".
Kisiwa hiki kina historia ndefu ya ukaaji
wa bin'adam wenye ustaarabu wa
kipekee wanaojishughulisha na ukulima
mdogomdogo wa mazao ya mpunga,
minazi, migomba (ndizi), muhogo,
maharagwe-mekundu; pamoja na uvuvi
wa asili kwa utumizi wa mashua na
ngarawa (kwa mishipi, madema, ndoana
na mitego). Pemba inasifika sana kwa
kuwa na maeneo mazuri ya kupiga-
mbizi, matumbawe yasiyoharibiwa na
maisha mororo ya bahari kwa viumbe
na/au mimea wa/ya baharini (samaki,
kasa, majongoo, makonokono,
matumbawe, na mwani).
Mji Mkuu wa Kisiwa cha Pemba ni
Chake-Chake uliyopo juu ya
‘kilima' ilhali magharibi yake
kuna kisiwa kidogo cha Misali ambapo
mawimbi-bahari hutoa fursa ya wakati
gani ngalawa na/au mashua zinaweza
kuingia ghatini. Magharibi mwa Chake-
Chake kuna mkono-bahari maarufu wa
Mkumbuu uliyosheheni magofu (mabaki
ya majengo) ya Ndagoni yanayokadiriwa
kujengwa karne ya 14. Mashariki mwa
Mji wa Chake-Chake kuna magofu ya
Mkama Ndume yanayopatikana kwenye
kijiji cha Pujini (kusini ya uwanja wa
ndege). Magofu ya "Ngome ya Mkama
Ndume", kama yanavyojulikana,
yanakadiriwa kuwa ya kwanza katika
pwani yote ya Afrika Mashariki
yanayokadiriwa kujengwa na Wareno
mnamo karne ya 15.
Kisiwa cha Pemba kinasifika kwa
maeneo tajiri ya uvuvi wa samaki wa
baharini. Kati ya kisiwa hicho na
mwambao wa mkoa wa Tanga kuna
upana wa kama kilometa 32 za Mkondo
wa Pemba wenye utajiri mkubwa kwa
uvuvi katika pwani ya Afrika ya
Mashariki. Wakati wa "enzi za karafuu",
mapato ya Zanzibar (Pemba na Unguja)
yalitegemea sana zao la karafuu kwa
uchumi; na sehemu kubwa ya kilimo cha
karafuu (mashamba ya mikarafuu)
yalikuwapo/yangalipo kisiwani Pemba
(kama mikarafuu milioni 3.5 hivi) kwa
vile hali ya mazingira (udongo, mvua,
jotoridi na mwinuko) ya kisiwa hicho
inaruhusu ukulima na ustawishaji wa
zao la karafuu.
Pamoja na uzuri wa mandhari ya kisiwa
cha Pemba kijiografia na kimeteorolojia,
makala haya yamekuja si kuonesha uzuri
wa harufu ya marashi ya karafuu,
hasha! Makala haya yanajaribu kwa
muhtasari kuonesha kutengwa kwa
kisiwa cha Pemba tangu zama za
historia ya kabla ya yale yanaoitwa leo
"mapinduzi matukufu" ya tarehe 12
Januari 1964.
Pemba ni kisiwa; wala si ule Mji Mkuu
wa Jimbo la Cabo Delgado (Msumbiji) au
ule Mji Mdogo uliyopo nchini Zambia!
Pemba ni kisiwa wanachoishi wale leo
wanaoitwa Wapemba – watu
wanaopatikana kisiwani, wenye asili ya
kisiwani na waliyostaarabika na
Uswahili wa Pemba. Wanahistoria wengi
waliyoandika historia ya kisiwa cha
Pemba wanakinasibisha kisiwa hicho na
mchanganyiko wa watu wenye asili ya
Uarabu na Uswahili (mchanyato wa
Uarabu na Ubantu).
Wareno walikuwa wa kwanza kukikalia
kisiwa hicho na watu wake (Wapemba
wa kale) kwa mabavu hadi pale
walipotimuliwa na Imam Sultan bin Seif
mwaka 1652. Na kuanzia hapo, yaani
mwaka 1652, visiwa hivyo, yaani Pemba
na Unguja vikawa chini ya "Milki ya
Sultan wa Oman". Waarabu walipofika
maeneo ya visiwa hivyo waliwakuta
wenyeji wa huko (weusiweusi) na ndipo
walipoliita eneo hilo la visiwa kama
Zinji-bar (kwa Kiarabu) au Zang-bar
(kwa Kifursi).
Baada ya kuwashinda Wareno, Imam
Sultan bin Seif hakuanzisha maskani
yake visiwani humo bali aliondoka
kurejea Oman (Maskati) na alimuweka
mtu kutoka kwa ukoo wa Al'hath ili
aangalie ‘milki' yake mpya!
Alipofariki Imam Sultan bin Seif,
mamlaka ya kuendesha shughuli za dola
aliyashika mwanawe wa kiume, Seif bin
Sultan ambaye alikuwa mtawala
mwenye makeke na anayependa sifa za
kutawala; naye ndiye aliyekuwa
Mwarabu wa kwanza aliyeweza
kuzuiwiya "mauwaji holela" yaliyokuwa
yanafanywa na Wareno dhidi ya watu
weusi wa Afrika ya Mashariki.
Mwaka 1711, mjukuu wa Seif bin Sultan
aliachia ngazi baada ya kupoteza
udhibiti wa kuendesha dola na mahala
pake kuchukuliwa na ukoo wa Al'Busaid
na hawa masultan wa ukoo wa Al'Busaid
ndio waliyokuja kuwa masultan wa
Zanzibar kwa muda mrefu katika
historia.
Seyyid Said bin Sultan bin Ahmed
(aliyetawala kati ya 1804 na 1856)
alikuwa ni mjukuu wa Ahmed bin Said,
kiongozi wa kwanza wa ukoo wa
Al'Busaid aliyechukuwa usultan baada
ya kumuuwa ami ya baba yake (Badar
bin Seif) mwaka 1804 aliyetawala baada
ya kifo cha Seyyid Sultan. Mnamo
mwaka 1832, Seyyid Said alifanya
maamuzi ya kuhamisha makao makuu
ya ‘milki' yake kutoka Maskati
(Oman) na kuufanya Mji Mkongwe
(Unguja) kuwa ndiyo Mji Mkuu wa Milki
ya Usultan wa Oman. Uamuzi huu
uliigeuza Zanzibar (Unguja) katika
nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii
Dhamira ya Seyyid Said ilikuwa ni
kuubadilisha Mji wa Zanzibar (Unguja)
kuwa mji wa kibiashara mashariki ya
duniya. Uamuzi huo unatokana na
ukweli uliyokuwapo wakati huo kwamba
Unguja (Mji wa Zanzibar) ulikuwa na
ulinzi asilia wa matumbawe uliyozuwiya
mashambulizi ya adui kutokea baharini;
pamoja na kuwa na kina (kilindi) kirefu
cha bahari kinachotoa fursa kwa meli
kubwa kutia nanga, vilevile ugavi
muruwa wa maji safi (baridi) ya kunywa
kwa min'ajili ya wafanyabiashara na
meli zinazotia nanga Mjini Zanzibar.
Seyyid Said aliubadilisha Mji wa
Zanzibar (Unguja) kutoka nyumba za
udongo zilizoezekwa makuti (ya mnazi)
hadi kuwa wa maghorofa (na maroshani)
yaliyojengwa kwa mawe, chokaa na
zege. Ujenzi wa nyumba ulifanywa na
mafundi stadi na makini kutoka
Uarabuni na kusaidiwa na vibarua wa
kizalendo. Maendeleo haya ya haraka ya
Mji wa Zanzibar yaliwashajihisha
Waomani wengi kuhama kutoka Oman
na kuja kuishi Mjini Zanzibar.
Seyyid Said alianzisha "Biashara ya
Kubadilishana" na Wazungu
waliyowekeza kwenye fukwe za
Zanzibar. Katika kufikia malengo yake,
Seyyid Said aliwashajihisha wageni
(Wazungu) (kama wanavyofanya sasa
watawala wa kimamboleo) kufungua
vituo vya biashara kisiwani Unguja
(Zanzibar), na mwaka 1833 alisaini
"Mkataba wa Biashara" na Wamerekani
kuanzisha biashara katika ‘milki'
yake. Waomani walibadilishana bidhaa
kama nazi, magamba ya kobe (kasa),
pilipili nyekundu, nta na bidhaa
nyengine zilizopatikana wakati huo na
kwa upande wa Wamerekani
waliwaletea vifaa vya ujenzi, pamba,
sufi na nyuzinyuzi za nguo.
Kutokana na "Mkataba wa Biashara"
uliyosainiwa, Wamerikani walianzisha
wakala wa biashara Zanzibar (Unguja
Mjini) aliyejulikana kama John Berthram
& Co (kutoka Salem Massachusetts) na
baadaye mwaka 1837 Marekani
ilifungua rasmi ubalozi wa kwanza
visiwani Zanzibar – makao ya
ofisi za ubalozi yalikuwa Mjini Zanzibar!
Kutokana na kupanuka na kunawiri kwa
biashara, kampuni lingine la kibiashara
la Arnold Hines & Co (kutoka New York)
likafungua ofisi Mjini Zanzibar. Kana
kwamba si Wamarekani peke yao, bali
pia mwaka 1841 Uingereza ikafungua
ofisi ya kampuni ya kibiashara
iliyofuatiwa na kuweka ofisi ya ubalozi
(consulate) Mjini Zanzibar. Baadaye,
nchi za utaliano, Ujerumani, Ubeleji,
Ufaransa, na Austria zilituma "ujumbe"
wao Zanzibar ili kuangalia fursa
zilizopo na kuweka vituo vyao. Zanzibar
(Unguja) ilianza kuingizwa kwenye
mawanda ya diplomasia ya kimataifa
kutokea Mji Mkongwe (Unguja) ilhali
Pemba (kisiwa) kikiachwa solemba!
Utashi wa Seyyid Said katika kukuza
kilimo cha kibiashara kulipelekea
kuvumbua matumizi ya ardhi yenye
rutuba ya visiwa vya Pemba na Unguja.
Seyyid Said alianza "utafiti" wa kutafuta
zao (mmea) litakolopewa thamani na
Wazanzibari na kuvuta soko la
ulimwengu. Jibu la "utafiti" wake likawa
ni mmea (au zao) wa karafuu
uliyopatikana kutoka visiwa vya
Moluccus ambao maua yake yakikauka
huwa na harufu ya viungo kwa jina
karafuu.
Seyyid Said alinunua miche kwa maelfu
kutoka Moluccus na kuwashajihisha
wakulima (wengi wakiwa Waarabu kwa
wakati huo) kupanda miti ya karafuu
kwa wingi! Karafuu ya Zanzibar ilikuwa
bora sana kwa vile ililimwa kwenye
ardhi yenye rutuba na hali-bora ya
hewa. Ukulima mkubwa wa zao (mmea)
hilo ulikuwa zaidi kisiwani Pemba
– kwa hiyo Pemba kukawa
mashamba zaidi ilhali Unguja (mjini)
kukawa mjini zaidi kwa shughuli za
kiserikali, kidiplomasia, kiuchumi na
kijamii.
Wakati wa utawala wake Seyyid Said
alikienda mara kwa mara "nyumbani
kwao – Oman" kutatua mizozo ya
kisiasa ya ndani; na mwaka 1856 wakati
akirejea kutoka Oman alipatwa na
maradhi yaliyopelekea kifo chake akiwa
"chomboni" tarehe 19 Oktoba 1856 nje
kidogo ya visiwa vya Ushelisheli. Baada
ya kifo cha Seyyid Said alitawala mtoto
wake mdogo wa kiume, Seyyid Majid
Said bin Sultan (aliyetawala kati ya
mwaka 1856 hadi 1870) alichukuwa
usultan badala ya kaka yake Thuwain.
Thuwain alijaribu kutaka nafasi ya
usultan (wa Zanzibar) hata hivyo
Uingereza ambayo ilikuwa "mlinzi"
iliteuwa Tume ya Canning kutatua
mzozo huo.
Uingereza ilimpendelea Majid na wakati
huohuo iliweza kumpoza Thuwain.
Uamuzi ulikuwa kwamba Thuwain
atawale Oman na maeneo ya pembe ya
Afrika (Djibuti, Eritrea na Somaliland)
na Majid atawale Zanzibar. Uamuzi huu
ulianzisha tawala mbili ndogo chini ya
"Milki ya Usultan wa Oman" na kuweka
mifumo ya utawala na mahakama
ilipofika mwaka 1861.
Mfumo huu wa utawala ulisababisha
mizozo kati ya Majid na kaka yake
Bargash; na Uingereza kama kawaida
yake iliingilia kati na kumpeleka
Bargash Mumbai (Bombay) nchini India
kwa masomo zaidi. Baada ya kifo cha
Majid, Barghash alirejea Zanzibar akiwa
na uchu, hamu na ghamu ya kuchukuwa
utawala ili kuonesha utashi wake wa
kuyaenzi maisha ya kimagharibi na
kifahari aliyoyapata alipokuwa
masomoni nchini India. Kwa mtaji huo,
Seyyid Barghash alitumia fedha nyingi
kwa maendeleo ya usultan wake
– aliwezesha kusambaza maji ya
bomba (mfereji) kutoka kwa chechem ya
asili hadi Mjini Zanzibar!
Mwaka 1872, Seyyid Barghash
alilishawishi kampuni la meli la India la
British India Steam Navigation Company
kuanza huduma za kila mwezi za usafiri
wa meli kati ya miji ya Aden na
Zanzibar. Huduma hii iliiwezesha
Zanzibar kusafirisha barua na vifurushi
sehemu mbalimbali za dunia. Baada ya
kufunguliwa kwa Mfereji wa Suez
(mwaka 1869), Seyyid Barghash aliingia
mkataba na kampuni la Eastern
Telegraphic Company kutandaza mkonga
wa mawasiliano ya simu chini ya bahari
kati ya Aden na Zanzibar! Kazi ya
kutandaza mkonga huo wa chini ya
bahari ilimalizika mwaka 1879 na ofisi
ya mawasiliano ya simu ilifuguliwa
kukiwa na wataalamu na mafundi sanifu
kutoka Uingereza, Goa na Mumbai
(Bombay) – India.
Inasemekana kwamba Seyyid Said
alikuwa kinara wa kuzuiya biashara
haramu ya utumwa pale alipotiliana
saini na Uingereza wa kuizuwiya
biashara hiyo mwaka 1870; hii ilifuatiwa
na kuzuwiya biashara hiyo kwenye
‘milki' ya Zanzibar na kulifunga
"Soko la Watumwa" lililokuwapo
Mkunazini (mahala palipojengwa Kanisa
la Kiingereza – Anglican Church).
Seyyid Barghash alikufa mwaka 1888
kutokana na utu uzima na msongo wa
kuongoza ‘milki' yake.
Kifo cha Seyyid Barghash kilimleta
kwenye kiti cha usultan Seyyid Khalifa
aliyeendeleza yale ya Barghash hususan
kuzuia biashara haramu ya utumwa na
yeye (Khalifa) alitoa amri kwamba
"watumwa wote watakaoingia kwenye
milki yake wataachwa huru". Seyyid
Khalifa alikufa kwa "homa" akiwa na
umri wa miaka 36 tarehe 13 Februari
1890 akitawala miaka miwili tu!
Baada ya Seyyid Khalifa alifuatia Seyyid
Ali bin Said. Seyyid Ali bin Said aliiweka
Zanzibar na Pemba chini ya "Ulinzi wa
Uingereza" mnamo tarehe 1 Novemba
1890. Katika kipindi hichohicho kifupi
alichotawala Seyyid Ali bin Said
alitawala vilevile Seyyid Hemed bin
Thuwein (yaani kati ya mwaka 1890
hadi 1893). Wote hawa walikuwa na
maskani yao Mjini Zanzibar!
Seyyid Khalid bin Barghash alichukuwa
utawala wa Zanzibar kwa "nguvu"
mnamo tarehe 25 Agosti 1896 kinyume
na utashi wa Uingereza waliyomtaka
Seyyid Hamoud. Khalid bin Barghash
alipewa muda maalumu wa
kujisalimisha kwa Uingereza,
aliposhindwa meli za kivita za Uingereza
zilizokuwa chini ya amri ya Rear
Admiral Rawson zililishambulia "Jumba
la Kisultan" kwa mizinga; na kuhofia
usalama wake Khalid bin Barghash
alikimbilia Dar es Salaam na kuomba
hifadhi kwa serikali ya Ujerumani
iliyokuwa inatawala Tanganyika wakati
ule.
Baada ya kukimbia kwa Khalid bin
Barghash Uingereza harakaharaka
ikamuapisha Seyyid Hamoud kuwa
Sultan wa Zanzibar. Seyyid Hamoud
alikuwa na mtoto mmoja wa kiume
aliyekiitwa Ali aliyesomeshwa Uingereza
katika Chuo Kikuu cha Harrow. Seyyid
Hamoud alikufa tarehe 18 Juni 1902
akiwa na umri wa miaka 51 baada ya
kifo cha rafiki yake mpenzi na msiri
wake mkuu, Sir Lyod Mathews aliyekufa
mwaka 1901.
Wakati wa kifo cha Seyyid Hamoud, Ali
alikuwa mtoto (kijana) mdogo.
Alipopewa kiti cha usultan aliishi maisha
ya kimagharibi kama alivyozoweya
alipokuwa akisoma Uingereza. Mwaka
1911 alikaribishwa kuhudhuria "Sherehe
za Kuwekwa Wakfu wa Ufalme" Mfalme
George wa IV. Alipokuwa Ulaya aliamua
kukitelekeza kiti cha usultan na kubaki
Ulaya! Katika mazingira ya kutatanisha
alifariki akiwa Ufaransa katika mwaka
huohuo (wa 1911). Watoto wake
waliyobaki Zanzibar hawakuhitaji kiti
cha usultan alichokiacha baba yao!
Nafasi iliyoachwa wazi na Seyyid
Hamoud ilichukuliwa na Seyyid Khalifa
bin Haroub na "Ulinzi wa Uingereza"
uliondolewa kutoka Ofisi ya Mambo ya
Nje na kupelekwa kwenye "Ofisi ya
Makoloni" mwaka 1925. Ofisi ya Ubalozi
na Wakala wa Ufalme (Consulate and
Majesty Agency) ilibadilishwa na nafasi
ya Balozi wa Uingereza Mkazi iliundwa.
Katika kipindi hiki bandari ya Zanzibar
ilipanuliwa na kuwekwa zana na vifaa;
barabara za lami zilijengwa kuzunguka
maeneo muhimu ili kurahisha biashara.
Vilevile, elimu na huduma za afya
zilibuniwa na kupanuliwa hadi
mashambani! Mfumo wa sheria
uliboreshwa kwa kuweka mabaraza ya
wenyeji (native councils) na mahakama
za mudir zilianzishwa. Seyyid Khalifa
bin Haroub alifariki Oktoba 1960. hata
wakati wa kifo cha Sultan Seyyid Khalifa
bin Haroub alikuwa akiishi Mjini
Zanzibar!
Nafasi ya Khalifa bin Haroub ikachuliwa
na Seyyid Abdullah bin Haroub. Hata
hivyo utawala wake ulikatishwa na kifo
kilichotokana na hali mbaya ya afya
yake. Alikiugua "kisukari" kwa muda
mrefu hali iliyopelekea kuvimba kwa
"gangrene" na kusababisha miguu yake
ikatwe. Seyyid Abdullah bin Haroub
alifariki mwaka 1963 alipokuwa
anafanyiwa upasuaji wa kukata miguu
yake!
Na wa mwisho katika silsila ya usultan
wa Zanzibar alikuwa Seyyid Jamsheed
bin Abdullah. Jamsheed bin Abdullah
alikuwa mtoto wa Seyyid Abdullah bin
Haroub; alipata elimu yake kwenye Chuo
Kikuu cha Kijeshi cha Naval Academy,
Uingereza kama wanavyosoma watoto
wengi wa familia za kifalme na/au
kisultani. Seyyid Jamsheed bin Abdullah
alimrithi baba yake tarehe 1 Julai 1963.
Kama baba yake, utawala wake haukuwa
mrefu na aliondolewa na "mapinduzi"
yanayoitwa matukufu ya tarehe 12
Januari 1964! Jamsheed bin Abdullah
alifanikiwa kutoroka kwa kutumia
mashua binafsi (Al Hathira) hadi Dar es
Salaam na alipewa "hadhi" ya ukimbizi
wa kisiasa nchini Uingereza.
Masultan wote tuliowasoma na
kuwaelezea hapa walielekeza nguvu zao
kiuchumi, kisiasa na kijamii katika
kuijenga Zanzibar Mjini (Unguja) na
kuiacha Pemba pembeni. Hata yale
mapinduzi ya tarehe 12 Januari 1964
yaliyoandaliwa na "Field Marshal" John
Okello (Messiah Mjinga) yaliendeleza
hali hiyo ya kukitenga kisiwa cha Pemba
na Wapemba sawiya!
Upembuzi na udondozi wa kihistoria wa
kutengwa kwa kisiwa cha Pemba ndio
chimbuko la "mpasuko" wa kisiasa
unaoendelea leo visiwani humo. Historia
inaonesha kwamba: palikuwapo na ZPPP
(Zanzibar and Pemba Peoples Party) na
ZNP (Zanzibar Nationalist Party)
vilivyoungana mwaka 1961 na kuunda
umoja wa Waafrika weusi (wengi) na
Waarabu (wachache) waliyokilazimisha
chama cha ASP (Afro-Shirazi Party) kuwa
chama cha upinzani! Ngome ya ZNP
ilikuwa Pemba – na hili ndilo
chimbuko la kuendeleza "chuki"
inayotokana na "mapinduzi daima"
yaliyoasisiwa na "mhandisi, mhunzi,
fundi-mchundo" wa mapinduzi
aliyeshirikiana na baadhi ya mamluki
waliyokodiwa kuendesha mauwaji ya
watu kati ya 15,000 na 25,000 wengi
wakiwa wenye asili ya Kiarabu, Kihindi
na Kifursi.
John Okello alipanda mbegu ya chuki
kati ya Wapemba na Waunguja na
kutengeneza "upogo" uliyojengwa
kwenye misingi ya ubaguzi wa rangi (na
dini); japokuwa wapo watu wa Unguja
wanaojiita Waislam ilhali vitendo vyao
ni kinyume navyo. Kuundwa kwa CCM
(kulikotokana na kuunganishwa kwa ASP
na TANU) ilikuwa njama mahsusi ya
kuviingiza visiwa vya Pemba na Unguja
katika mfumo wa Kimarekani na
kuondoa satwa ya Waingereza
waliyokuwa nayo kabla ya tarehe 10
Desemba 1963 siku ya Uhuru wa
Zanzibar na kufuatiwa na mapinduzi
yaliyofanywa kwa madai ya kuondoa
usultani wa ki-Oman na kuweka usultani
wa tabaka la wanaojiita
"wanamapinduzi" – wenye uchu
na tamaa ya kuendeleza kumwaga damu
za watu wasiyo na hatia.
Kama Wapemba (na kisiwa cha Pemba)
walitengwa kijamii, kiuchumi na kisiasa
tangu mwaka 1652, sioni sababu kwa
nini Pemba isijitenge!
Hii inatosha kuonesha utengano uliyopo
& ni ufa gani unaotakiwa uzibwe
kama hali ni hii kwa zaidi ya miaka
350? Matokeo ya songombingo na/au
sintofahamu ya kisiasa, kijamii na
kiuchumi kwa kipindi cha miaka kati ya
1652 na 2014 inatosha kuonesha
kutengwa kwa kisiwa cha Pemba. Na
kama ipo nia ya dhati kwa yeyote
anayejifanya mkombozi (na/au mtatuzi)
wa kutafuta tiba mujarabu ya mpasuko
wa kisiasa visiwani Unguja na Pemba;
basi na aitazame upya historia ya
mpasuko huo na nini chanzo chake kisha
aelekeze "nguvu" za ziada katika
kulivunja "genge" la wahafidhina wenye
ubaguzi ndani ya CCM-Zanzibar.
Inawezekana, ni uamuzi makini
unaohitajika kuukubali ukweli wa
"Mpasuko wa Zanzibar" na utashi wa
kisiasa kuutatua unaohitajika. Viongozi
wa CCM (Bara na Zanzibar) waache
unafiki, unazi, uzabizabina, uzuvendi,
undava, na undumilakuwili wakubali
ukweli juu ya suluhisho hilo.
Naomba maoni yako na msaada juu ya majalada yangu pia naomba ufuatilie machapisho yajayo.
Wako mwana sanaa mchanga wa historia          Yahya El~Nabahaniy.
                                  MWISHO
                               Ahsante sana

Maoni

Machapisho Maarufu