Historia ya maisha ya Ali Hassan Mwinyi

HISTORIA YA MZEE RUHSA
ALHAJJ ALI HASSAN MWINYI
Mwandishi :Yahya Makamo
LEO KATIKA HISTORIA:  TUMJUE  "MZEE WA RUKHSA" RAIS MSTAAFU ALI HASSAN MWINYI

Ali Hassan Mwinyi alizaliwa tarehe 8 mwezi wa tano (Mei) mwaka 1925 katika kijiji cha Kivure, wilayani Kisarawe ,mkoa wa Pwani, Tanzania Bara. Kama wengi wa viongozi wetu, Mwinyi naye alizaliwa katika iliyokuwa Tanganyika. Akiwa bado mwenye umri mdogo sana familia yake ilihamia Zanzibar. Kwa maana hiyo Mwinyi ni mzaliwa wa bara aliyekulia na kuendelea kuishi visiwani Zanzibar.

Alianza safari yake kielimu huko visiwani Zanzibar katika shule ya msingi Mangapwani kuanzia mwaka 1933 hadi 1936 kabla ya kujiunga na shule ya sekondari Dole kwa ajili ya elimu ya sekondari kuanzia mwaka 1937 mpaka mwaka 1942. Baada ya hapo alijiunga na Chuo Cha Ualimu Zanzibar kusomea ualimu kuanzia mwaka 1943 mpaka 1944.

Kuanzia mwaka 1945 mpaka mwaka 1950 alirejea tena katika shule ya Mangapwani,shule aliyosomea,safari hii akiwa sio mwanafunzi tena bali Mwalimu.Kuanzia mwaka 1950 mpaka 1954 alikuwa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo wakati huo huo alikuwa akiongeza elimu yake kwa kujipatia General Certificate in Education (GCE) na pia aliendelea kusoma chuo cha Durban University Institute of Education, United Kingdom kusomea stashahada ya ualimu.
Baada ya hapo alijiunga tena na Chuo Cha Ualimu Zanzibar kama mkufunzi kuanzia mwaka 1956 mpaka mwaka 1961 Pia alirudi Regent Institute kilichopo London nchini Uingereza ambapo alijipatia cheti cha ufundishaji lugha ya kiingereza.

Kuanzia mwaka 1961 mpaka 1962 alijiunga na Hall University, Uingereza katika Tutors’ Attachment Course. Mzee Mwinyi pia ana cheti ya lugha ya kiarabu alichokipatia Cairo nchini Misri kati ya mwaka 1972 na 1974.

Safari yake ya kisiasa aliianza rasmi mwaka 1964 alipojiunga na Afro Shiraz Party (ASP) huko Zanzibar ambapo alikitumikia chama katika ngazi na nafasi mbalimbali.
Kati ya mwaka 1964 na 1965 alikuwa ni Katibu Mkuu wa muda katika wizara ya elimu Zanzibar kabla hajateuliwa kuwa Naibu Mkurugenzi katika iliyokuwa Zanzibar State Trading Corporation (ZSTC).
Hiyo ilikuwa ni kati ya mwaka 1965 na mwaka 1970. Pia katika miaka hiyo hiyo, kuanzia mwaka 1966 mpaka 1970, Mwinyi alikuwa mweka hazina msaidizi katika tawi la ASP la Makadara,Zanzibar. Wakati huo huo pia kati ya mwaka 1964 mpaka 1977 alikuwa ni mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA)

Majukumu mengine aliyokuwa nayo miaka hiyo ni pamoja na uenyekiti wa Zanzibar Censorship Board (1964-1965), Mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam na pia mwenyekiti wa Baraza la Chakula na Lishe.

Kuanzia mwaka 1972 mpaka 1975, Mwinyi alikuwa ni Waziri wa Afya wa Tanzania kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kuanzia 1975 mpaka 1977. Mwaka 1977 aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri cheo alichokitumikia mpaka mwaka 1982 aliporejea nyumbani na kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii cheo ambacho alikutumia kwa muda mfupi tu kwani mwaka 1983 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi katika ofisi ya Makamu wa Raisi.

Mwaka 1984, kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Raisi wa Zanzibar wakati huo,Alhaj Aboud Jumbe, Mwinyi alichaguliwa kuwa Raisi wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar na wakati huo huo Makamu wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kuanzia mwezi August mwaka huo huo wa 1984 Mwinyi alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi cheo alichoendelea nacho mpaka mwaka 1990 baada ya kung’atuka kwa Hayati Mwalimu Nyerere kutoka katika kukiongoza Chama Cha Mapinduzi(CCM)

Mwalimu Nyerere aliamua kung'atuka kwa hiari yake na kumuachia kwa njia ya kidemokrasia madaraka ya urais Alhaji Ali Hassan Mwinyi. Hiyo ilikuwa mnamo 1985.

Alipoingia madarakani kumpokea aliyekuwa Raisi wa Awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Nyerere mnamo tarehe 5 Novemba mwaka 1985, watanzania wachache sana (kama wapo) waliweza kutabiri kwamba miaka kumi baadaye na zaidi baada ya kustaafu rasmi, ataibuka kuwa mmojawapo wa maraisi wa Tanzania ambao watabakia kupendwa na kuheshimika kwa namna ya kipekee kabisa.

Tunadiriki kusema “namna ya kipekee” kwa sababu ukweli unabakia kwamba inapofanyika tathmini ya uongozi wake, bado mtu au watu mbalimbali wanakuwa na maoni yao tofauti tofauti kuhusiana na suala hilo. Utoaji huo wa tathmini ni suala ambalo haliwezi kukoma leo wala kesho, ni tukio linaloendea na litakaloendelea, vizazi mpaka vizazi.

Mwinyi kihistoria na utawala wake.

Huo ndio uzuri au ubaya wa historia na muda (history and time),huwa vina jinsi ya kipekee katika kutoa hukumu zao.

Mpaka anakabidhi madaraka yake ya uraisi kwa raisi wa awamu ya tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa mnamo tarehe 23 November mwaka 1995, jina ambalo wengi tulipenda kulitumia ni “Mzee Rukhsa” ingawa kamwe hatukuwahi kusahau kwamba jina lake kamili ni Ali Hassan Mwinyi, Raisi wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Kihistoria, Ni wakati wa Uongozi wake ndipo mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa!

Rais Msaafu wa awamu ya pili Mh. Ali Hassan Mwinyi ni mtaalamu wa lugha ya Kiswahili na pia hupenda michezo hususani jogging. Mwinyi ameoa wake wawili (Sitti Mwinyi na Khadija Mwinyi), ana watoto na wajukuu. Anaishi Msasani jijini Dar-es-salaam.

Maoni

  1. Shukurani zangu zimwendee mzee mwinyi kwa kazi nzuri alizo zifanya.

    JibuFuta
  2. kila la kheri mzee wetu mwinyi kwa kazi kubwa uliowafanyia wa Tanzania

    JibuFuta
  3. kila la kheri mzee wetu mwinyi kwa kazi kubwa uliowafanyia wa Tanzania

    JibuFuta
  4. Duh kumbe mzee kasoma ivo nilikua cjui kabsa

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Machapisho Maarufu